Mwanzo > Habari Mpya za ubalozi wa China
Hadhi Bandari ya Dar haitabadilika'
2014/01/28
 

By Mwananchi Jan.27th

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu amesema pamoja na kujengwa kwa bandari kubwa ya Bagamoyo, hadhi ya Bandari ya Dar es Salaam itabaki kama ilivyo.

Dk Nagu aliyasema hayo juzi usiku alipokuwa akizungumza katika sherehe za Mwaka Mpya wa China zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, waziri huyo alikuwa akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

"Naipongeza Serikali ya China kwa kukubali kujenga Bandari ya Bagamoyo, lakini sifa na hadhi ya Bandari ya Dar es Salaam haitabadilishwa," alisema Dk Nagu.

Alisema sherehe hizo zilizofanyika kwa mara ya tano nchini, zimesaidia kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na China na hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa bomba la gesi ya Mtwara, ujenzi wa Uwanja wa Taifa na kadhalika.

Balozi wa China nchini, LU Youqing, alisema kutokana na uwekezaji huo, China imekuwa ya pili kwa uwekezaji nchini Tanzania ikiwa na miradi ya Dola 2.17 bilioni na kutengeneza ajira zaidi ya 100,000.

Balozi Youqing alisema ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China, umeimarika hadi kufikia Dola2.5 bilion na kwamba kuna fursa za biashara zaidi ya 350,000 kwa Watanzania.

"Uwekezaji wa China katika Tanzania utasaidia ukuaji wa uchumi, kuboresha maisha na tunataka kuona Tanzania inapiga hatua za kiuchumi," alisema balozi huyo.

Alielezea matumaini yake kuwa uhusiano mzuri kati ya nchi hizi mbili utaendelea kudumishwa kwa manufaa ya watu wake.

 

Suggset To Friend:   
Print