Mwanzo > Habari kuhusu China
DK Shein asifu ushirikiano wa China
2014-01-28 01:22
 

Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted  Jumanne,Januari14  2014  saa 24:0 AM

 

Zanzibar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Mjumbe Maalumu wa Rais Xi Jinping wa China na kujadili jinsi nchi hiyo inavyoweza kuchochea kasi ya maendeleo ya Wazanzibari.

Mjumbe huyo ambaye ni Waziri wa Makazi na Maendeleo wa Miji na Vijiji nchini China, Jiang Weixin aliwasili Zanzibar ili kumwakilisha Rais Xi Jinping katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ikulu ya Zanzibar, inaeleza kuwa Dk Shein alimweleza mgeni huyo kuwa katika miaka 50 ya Mapinduzi China imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na watu wa Zanzibar katika harakati zao za kujiletea maendeleo.

Alitolea mfano ushirikiano wa Zanzibar na China mara baada ya Mapinduzi ambapo nchi hiyo ilisaidia katika uanzishwaji wa viwanda mbalimbali, misaada katika kuendeleza kilimo cha kisasa, michezo, sekta ya habari pamoja na uimarishaji wa sekta ya afya ambayo ilikuwa nyuma sana humu nchini.

Aliongeza kuwa kwa Zanzibar kuzungumzia maendeleo ya sekta ya afya haiwezekani bila ya kutambua mchango mkubwa Serikali ya watu wa China na wataalamu kutoka nchi hiyo ambao walianza kufanya kazi nchini mara tu baada ya Mapinduzi.

Katika mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Dk Shein alisema kitendo cha Rais Xi Jinping kumtuma Mjumbe wake Maalum kushiriki maadhimisho hayo ni uthibitisho wa urafiki wa kweli uliodumu kwa miongo mingi kati ya Serikali na wananchi wa nchi mbili hizo.

Alimweleza Mjumbe huyo kuwa wananchi wa Zanzibar wamefarijika sana kupokea salamu za kuwatakia heri katika maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi..

Alisisitiza kuwa kitendo cha Jamhuri ya Watu wa China kuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar kitabaki katika kumbukumbu za historia ya ukombozi wa watu wa Zanzibar.

Alieleza kuwa kitendo hicho hakiwezi kusahaulika kwa kuwa miaka 50 iliyopita wananchi wa Zanzibar walipokataa kutawaliwa na kuamua kujitawala wenyewe walihitaji kuungwa mkono na wanachi wenzao kote ulimwenguni na ndipo China bila ya ajizi ikayatambua Mapinduzi mara moja.

Dk. Shein alimueleza Mjumbe huyo Maalum wa Rais Xi Jinping kuwa ushirikiano kati ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla na Serikali na wananchi wa China umekuwa ukiimarika.

Kwa upande wake, Bwana Jiang alieleza kuwa ni heshima kubwa kwake kuwasilisha Salamu za Pongezi na za Kirafiki kutoka kwa Rais Xi Jinping na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na wananchi wa Zanzibar wakati huu wa kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi.

 

Suggset To Friend:   
Print