Mwanzo > Habari kuhusu China
Wafanyabiashara Tanzania, China wajengeana uwezo
2014-07-04 20:51

Dar es Salaam. Kongamano la biashara lililomalizika jana nchini limewawezesha wafanyabiashara nchini kukutana ana kwa ana na wenzao wa China, kubadilishana taarifa na kujenga mtandao wa kibiashara kwa faida yao na nchi kwa ujumla.

Pia, kongamano hilo lililofunguliwa na makamu wa rais wa China, Li Yuanchao limewawezesha wafanyabiashara wa nchi zote mbili kujenga hali ya kujiamini katika biashara baada ya kufahamiana.

Mafanikio ya mkutano huo wa siku tatu, yameelezwa na mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Juliet Kairuki kuwa ya muhimu kwa Taifa, hivyo akawataka wafanyabiashara wa Tanzania kutumia uhusiano walioujenga kujiimarisha kimataifa.

“Fursa hii ikitumika vyema itasaidia wafanyabiashara wetu kukua na hivyo kuongeza mapato katika nchi kwa kuvutia mitaji, teknolojia na ujuzi,” alisema.

Alisema wafanyabiashara wa China wapo tayari kufanya biashara na Watanzania ambao alisema wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo waliyoipata.

Mwenyekiti wa bodi ya TIC, Profesa Lucian Msambichaka alisema wawekezaji kutoka China wamekuja nchini kwa wakati mwafaka na ambao taifa linawahitaji.

“Tunatambua bila uwekezaji hakuna maendeleo ndiyo maana hata nchi nyingi duniani zinavutia wawekeji na mitaji,” alisema.

Mmoja wa wawekezaji kutoka China, Kendall alisema amefurahishwa na taarifa alizozipata katika kongamano hilo kuhusu Tanzania.

 

Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Juni26  2014 

Suggset To Friend:   
Print